Mpango wa kuanzisha sekondari kata ulipokewa kwa shangwe na wazazi wengi. waliamini kwamba watoto wao wangepata nafasi kubwa ya kuchaguliwa kujiunga na sekondari lakini pia wangesoma karibu na makwao.
Lakini inavyoeleweka, dhamira na malengo havifanani kabisa.Wanafunzi hao wameendelea kuchaguliwa kujiunga na shule zilizo mbali na makwao hivyo kuendelea au kuwaongezea adha ya usafiri.
Ndiyo maana baadhi ya wazazi wamefika mahali wanapohoji umuhimu wa shule za kata ambazo walizijenga wakiamini kwamba, zingetatua matatizo ya watoto walio katika maeneo yao kuondokana na adha ya usafiri na kupata elimu ya uhakika.
Hata hivyo kwenye usafiri hali ni mbaya na hakuna dalili ya lini itakuwa angalau nafuu kwa wanafunzi kama hao ambao hiari ya kusoma karibu na majumbani kwao haipo.
Ni kipindi kirefu tangu sasa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), ilipotangaza kuwafutia leseni na kuwachukulia hatua za kisheria madereva na makondakta wanaopatikana na makosa ya kuwanyanyasa wanafunzi.
Tangu Sumatra itoe ahadi hiyo hatujasikia hatua zilizochukuliwa na unyanyasaji huo unaoendelea hasa katika Jiji la Dar es salaam.
Kwa kifupi badala ya kupungua, tatizo hilo limekuwa likongezeka kwa kasi siku hadi siku.
Labda mamlaka hii imesahau kama maandalizi ya viongozi bora wa taifa hili siku za usoni ndiyo hao wanaopata adha ya usafiri. Kwanini shida hizi ambazo zinaweza kukomeshwa kwa amani bila vurugu zisifanyiwe kazi, ili watoto wetu wapate elimu bora kwa kuwahi vipindi?
Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa mamlaka hiyo na kuahidi kwamba angeshirikiana na jeshi la polisi upande wa usalama barabarani kwa kuwa kazi yao inahusisha usalama kwa wasafiri na vyombo vyao imeishia hewani.
Sumatra ilitoa ahadi hiyo wakati aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Abbas Kandoro alipokuwa akifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya mkoa wake mwishoni mwa mwaka jana, lakini sasa ni takriban mwaka sasa hakuna dalili zinazoonyesha hatua iliyochukuliwa.
Ni ukweli usiofichika kwamba bado wanafunzi wanataabika kutokana na usafiri na wengine wakiharibu na kupoteza nyenzo muhimu za kujifunza, ina maana viongozi wa mamlaka hii wamesahau kuwa ahadi ni deni?
Wahenga walisema haja ya nja hunena muungwana ni vitendo, katika hili la kutatua kero ya usafiri kwa wanafunzi Sumatra haina budi kukiri kwamba imewahadaa wanafunzi na kiungwana, iwaombe radhi.
Kwa mtazamo wangu, sera ya polisi jamii na ulinzi shirikishi inastahili kupelekwa kwenye upande wa usafiri wa wanafunzi labda hiyo itasaidia kwa kuwa viongozi wa pande zote mbili wataliangalia kwa umakini zaidi.
Kwa kuwa polisi imeshatuthibitishia kwamba sera hii imekuwa na mfanikio makubwa ambayo hata wengi wetu tunakubaliana nalo,tunaomba ligeukie katika hili la wanafunzi hasa kwa kuwa mpango wa shule za kata unaonekana kutolenga kuwaondolea adha hii ya usafiri lakini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inapaswa kurejea madhumuni ya kuanzishwa kwa shule hizi za kata ikiwa na jitihada za kuondoa kero hii ya watoto wetu kuhangaika kwenye mabasi na kupoteza muda wao mwingi wa masomo wakiwa njiani.
HAiyumkini mwanafunzi anayeishi Mbezi Luisi kwa mfano, kuchaguliwa kwenda kusoma Bunju na hii imeshatokea mara nyingi tu huku ikieleweka wazi kwamba hakuna usafiri unaounganisha maeneo hayo mawili.
Kwa maana hiyo mwanafunzi huyo analazimika kupanda basi hadi Ubungo kisha kuanza kutafuta usafiri wa kwenda huko. Tujiulize ataweza kweli kuhudhuria vyema masomo kwa maana ya kuwahi na kuzingatia kinchofundishwa?
Wizara inapaswa kutoa mwongozo wa manispaa husika kufanya uchambuzi yakinifu wa wanafunzi wote waonaochaguliwa kujiunga na sekondari hizi na kisha kuwapanga kwa kuzingatia maeneo wanakotoka.
Lakini wakatai tukisubiri hayo, Sumatra inapaswa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili la usafiri kwa wanafunzi hasa ikizingatiwa kwamba haijawahi kusema kwamba imeshindwa.
Sioni sababu ya Sumatra kushindwa kulitafutia ufumbuzi suala hili. Naamini vyombo hivi viwili vinaweza labda havijaamua tu au havijapata agizo na shinikizo kutoka juu.
Source: Mwananchi, makala imeandikwa na Ummy Muya 0715 33 66 41.
No comments:
Post a Comment