Tuesday, July 28, 2009

Maiti wa Ajali ya Tanga Watambuliwa!

WAKATI Jeshi la Polisi nchini likitangaza majina ya abiria waliokufa na waliojeruhiwa katika ajali ya basi la Mohamed Trans lililogongana uso kwa uso na lori wilayani Korogwe, mkoani Tanga, serikali imetoa takwimu zinazoonyesha kukithiri kwa ajali mbaya za barabarani nchini.
Akizungumza jana kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, James Kombe alisema kuwa watu waliothibitika kufariki kwenye ajali hiyo ni 28 na 14 kujeruhiwa. Hadi jana maiti 13 walikuwa wametambuliwa na miongoni ni ya mmoja wa madereva wa basi la Mohamed Trans, Joseph Kamitee.
Mwingine ni Ramadhani Kipsto, dereva wa lori lililohusika kwenye ajali hiyo linalojulikana kama Simba Track, ambalo lilikuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Arusha.
Wengine ni raia wawili wa Marekani akiwamo Catheline Brooke Baxter mwenye paspoti namba 089355273 iliyotolewa New Orleans na Francis Kanyoike, raia wa Kenya. Wote walikuwa wamepanda basi hilo lililokuwa linakwenda Dar es Salaam likitokea Mwanza kupitia Nairobi, Kenya.
Kombe aliwataja maiti wengine kuwa ni Hassan Ramadhani (35) Julius Mollel (40), Mkadara Saidi Athumani (32), Ludovic Mselle (48), Ainaini Maro (53), Wisdom Mmasa (17) na Ramadhani Shaaban (30).
Vilevile, aliwataja Baraka Shaaban (21), Mohamed Saidi Cheka (Utingo wa Lori), Hagilori Utrikari (43) mwenye asili ya Kiasia, Neema Robert (24), Helen Jamhuri (37), Mbaruku David Kassanda (35), Daniel Owino (34) na Cathyrin Brooke (32).
Maiti wote wamehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo baada ya kubainika kuwa majokofu katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, hayafanyi kazi ipasavyo.
Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gurumu la mbele la basi hilo kupasuka na kwa vile lilikuwa katika mwendo mkali, dereva alishindwa kulidhibiti na kwenda kuliparamia lori hilo lililokuwa linakuja mbele.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Rashid Said alisema majeruhi wawili wa ajali hiyo, hali zao zilikuwa mbaya na ilibidi wasafirishwe hadi Dar es Salaam ili wachunguzwe na kutibiwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Majeruhi hao aliwataja kuwa ni Maria Kika, mkazi wa Moshi na Mary Erasnos ambapo wote wamepata majeraha vichwani. Hata hivyo, alisema majeruhi ambao wataendelea kupata matibabu hospitalini hapo ni Erasmos Mathias, Nelson Giatu na Lugano Martin (mmoja wa madereva wa basi).
Majeruhi wengine ni Ahmed Abdallah (22) wa Nairobi, Abdallah Ademi (22), Peter Nyakua (43), Mtunzi Selemani(32, Mary Erasmus (27), Hellen Alex (23), Jane Njeri (33), Jenipher Mushi (29), Nelson Gitau (40), Jimmy Massawe (32) na Ludovic Mcharo.
Wakati huo huo, serikali jana ilitoa tamko ikisema kuwa licha ya ajali hiyo, tayari watu 1,468 walikuwa wamekufa na wengine 8,373 kujeruhiwa katika ajali 10,168 za barabarani zilizotokea nchini katika kipindi cha Januari na Juni, mwaka huu.
Tamko hilo lililosainiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha na kusambazwa kwenye vyombo vya habari jana, licha ya kusikitishwa na kasi ya wimbi la ajali hizo, lilitaja hatua kadhaa ambazo serikali imekusudia kuzichukua.
Masha alithibitisha kuwa katika ajali ya juzi iliyotokea Korogwe mkoani Tanga watu 28 walipoteza maisha, 18 wakiwa wanaume na 10 wanawake.
Alibainisha kuwa waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni14, kati yao wanawake watano na tisa ni wanaume. Masha alilalamika kwamba, ajali hizo zimeendelea kutokea licha ya serikali kutoa taarifa, maelekezo ya mara kwa mara na elimu kwa umma.
Alisema uchunguzi wa polisi unaonyesha kuwa ajali nyingi zinatokana na madereva wazembe wanaoendesha magari bila kuzingatia sheria za barabarani, hasa mwendo kasi. Kwa upande wa mabasi ya abiria, Masha alisema: "Chanzo chake kikuu ni pamoja na mwendo kasi, ubovu wa magari, uzembe wa wenye magari kwa kutoyakagua mara kwa mara, ulevi na makosa mbalimbali ya kibinadamu."
Pamoja na usugu huo wa madereva kutobadilika, Masha alisema kuwa serikali haijakata tamaa na itaendelea kuimarisha doria katika barabara kuu, ukaguzi wa magari ili kuyazuia mabovu na kuielimisha jamii ili itoe taarifa polisi wanapogundua dereva anaendesha vibaya.
Hatua nyingine alizitaja kuwa ni kuendelea kuboresha sheria za usalama barabarani, kuhimiza elimu kwa madereva, kukagua na kuhakiki uhalali wa leseni na kuwabana wamiliki wa magari ili waajiri madereva waaminifu na wanaowajibika katika kazi zao. Katika tamko hilo, Masha alitoa pole kwa wote waliopatwa na msiba pamoja na majeruhi katika ajali hiyo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Meja Jeneral Said Kalembo jana alizungumza na wananchi waliofika kwenye eneo la ajali hiyo na kuwatahadharisha kuwa wanaposafiri dereva akiendesha basi kwa mwendo wa kasi, watoe taarifa polisi ili waweze kudhibitiwa.
"Nawapa mkono wa pole ndugu wa waliokufa katika ajali hii, ni janga kubwa limetukuta Tanga, lakini nawaomba abiria mkiwa katika magari yanayoendeshwa kwa kasi toeni taarifa polisi," alisema Kalembo.
Naye Kombe alieleza kukerwa na mtindo wa baadhi ya madereva wa magari ya abiria kuendesha kwa kasi wakati wakijua wamebeba roho za watu. Mmoja wa majeruhi aliyejitambulisha kwa jina la Erasmus Mathias alisema ajali hiyo ilitokea baada ya tairi la la basi upande wa kushoto kupasuka na baadaye kulivaa roli na kisha magari yote yakaanguka.
"Dereva wa basi kama angekuwa amekwenda mwendo wa kawaida yasingetokea maafa kama haya," alisema Nasoro Juma, mkazi wa Kijiji cha Kwakombo.
Taken from: www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

This blog gives information about accidents-vehicles,motorcycles,bycycles etc,also highlights the suffering of those involved in various accidents. It gives counselling to the accidents victims and information as to where they can get assistance be it legal or humanitarian.
Health blogs
eXTReMe Tracker