Tuesday, August 18, 2009

Kiberenge Chagonga Daladala Dar Watu 23 Wajeruhiwa!

ZAIDI ya watu 20 jana walinusurika kifo katika eneo la kivuko cha reli kilichoko Barabara ya Mandela, Buguruni,baada ya kiberenge kugonga dalada iliyokuwa ikisanya abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Mbagala na Ubungo.
Tukio hilo lilitokea saa 2:00 asubuhi jana wakati dereva wa daladala hiyo aina ya DCM akijaribu kuvuka reli huku kiberenge kikipiga honi ya kuomba njia.
Hata hivyo daladala hiyo yenye namba za usajili T523 AGL, haikumudu kuvuka, jambo lililosababisha kugongwa na kiberenge.
Watu kadhaa walijeruhiwa katika tukio hilo ambalo walilielezea kuwa lilitokana na
uzembe wa dereva wa daladala.
Kwa mujibu wa majeruhi, kabla ya ajali abiria walimsihi dereva asubiri ili kupisha kiberenge kipite, lakini hakuwasikiliza.
Mmoja wa majeruhi hao, Rajabu Mkwachu (43) mkazi wa Mbagala, alisema alikuwa ameketi kwenye kiti kilicho karibu na mlango na ghafla alishitukia kiberenge kikilisukuma daladala kwa meta kadhaa kutoka katikati ya kivuko cha treni.
“Tulipwa nje ya barabara, nilipoteza fahamu na baadaye nilikuta nikiwa hapa Amana, nimeumia kichwani lakini nimepoteza fedha zangu Sh400,000 na simu aina ya Nokia yenye dhamani ya Sh280,000,”alisema Mkwachu.
Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo, pia walimshutumu dereva wa daladala kuwa ndiye kiini cha ajali hiyo, kufuatia kitendo chake cha kutokuwa makini, alipofika katika eneo la kivuko.
Waandishi wa habari hizi washuhudia baadhi abiria waliojeruhiwa wakitafuta mali zao bila mafanikio.
Daladala hiyo imeharibika vibaya na kuna madai kuwa dereva wake, aliruka wakati kiberenge kilipoanza kuburuza gari.

Katika harakati za kujiokoa akijaribu kukimbia mkazi wa Vingunguti Salum Shabani (30) aliyekuwa akinywa chai katika eneo la karibu na ajali, alivamia sufuria la moto la chai na kumsabaishia majeraha makubwa.
Majeraha hayo yako mapajani na mikononi.
“Nilikuwa nakunywa chai nikasikia sauti za watu wakilia huku wengine wakiwa wameshika vichwa na kukimbia hovyo. Kwa hiyo nami nikaona ni kherini nikimbie, ndipo nikaingia katika sufuria la chai nikaungua. Baadaye nililetwa hapa (Amana) kwa matibabu," alisema
Shabani
Martha Paulo (42) mkazi wa Mbagala ambaye ameumia kifua, mgongo na kiuno, alishindwa kupata matibabu ya haraka kutokana na kukosekana kwa huduma ya x-ray katika Hospitali ya Amana. Hali hiyo ilisababisha majeruhi huyo, kuhamishiwa Muhimbili.
Wengine walioumia ni pamoja na Maua Mohamed Mzee aliyeumia miguu,Abasi Mzee (26),victor Kweka na Julius Eusebio, ambao hali zao ni mbaya. Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Willy Sangu, alikiri kupokea majeruhi 23 wa ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment

This blog gives information about accidents-vehicles,motorcycles,bycycles etc,also highlights the suffering of those involved in various accidents. It gives counselling to the accidents victims and information as to where they can get assistance be it legal or humanitarian.
Health blogs
eXTReMe Tracker