Tuesday, August 18, 2009

Madereva wafuate sheria badala ya kuandaa mgomo

MADEREVA wa mabasi yaendayo mikoani wamesema wanaandaa mgomo mkubwa zaidi, kupinga adhabu aliyopewa dereva mwenzao, aliyehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, wakidai kuwa hailingani na kosa lake.
Madereva hao ambao katikati ya wiki iliyopita waligoma kwa masaa kadhaa wamedai kuwa wanaandaa mgomo huo kwa sababu wanapuuzwa na viongozi wa serikali; hivyo hiyo ni njia mojawapo ya kuishinikiza serikali kuisikiliza.
Zaidi ya hao wanadai kuwa wamechoka kunyanyaswa na askari wa usalama wa barabarani, ambao huwatoza fedha nyingi ambazo wanadai kuwa ni mradi wa baadhi ya wakubwa wa jeshi la polisi. Hii inaweza kutafsiriwa kwamba, askari wa usalama barabarani wanatumwa na wakubwa wao.
Ni dhahiri kuwa hatua wanayotaka kuchukua madereva hao inaathari kubwa kwa uchumi na usalama wa nchi, kwa sababu itasababisha abiria kutosafiri hivyo kuibua vurugu miongoni mwa jamii ambayo ni hatari kwa amani ya taifa.
Hivyo basi, pamoja na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuchukua hatua za kulipatia ufumbuzi suala hilo; ni muhimu juhudi zaidi zifanyike na mamlaka husika serikalini, kwa sababu mgomo huo unaweza kusambaa nchi nzima.
Si hivyo madai yao ya kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani yanahitaji kupewa kipaumbele kwa kuwa yana ukweli ndani yake, kwani ni ya muda mrefu; lakini yanaonekana kutopewa uzito, ndiyo maana askari wa usalama barabarani wanaendelea kudai rushwa bila aibu.
Hata hivyo, haipendezi kwa madereva kuchukua hatua ya kugoma kwasababu watawaumiza wananchi wasio na makosa na si vizuri kuwatumia wananchi kufanikisha madai yao. Kuna njia halali na za kisheria zinazoweza kutumika kupinga kifungo cha mwenzao ambacho wanaona hakutendewa haki.
Katika kudai haki ni vizuri kufuata utawala wa sheria, kwani kugoma hakuwezi kubatilisha sheria mpaka shinikizo lipite mahakamani na wanaotakiwa kufanya hivyo ni madereva kwa kukata rufaa kupitia kwa mawakili wao. Hivyo tunashauri wakatafute mawakili wa kuwasaidia kukata rufaa katika mahakama ya juu.
Ikumbukwe kuwa hukumu ya mahakama haitenguliwi na maandamano wala hoja za kisiasa au kwa amri ya mtu yeyote, bila kupitia mkondo wa sheria ambao hutolewa mahakamani.
Kwa maana hiyo, tunawaomba madereva wawe wavumilivu na wafuate utaratibu wa kisheria, ili waweze kupata haki yao kama inavyotokea katika baadhi ya hukumu zilizokatiwa rufaa na kubatilishwa mahakamani baada ya kubainika ilikosewa.
Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

This blog gives information about accidents-vehicles,motorcycles,bycycles etc,also highlights the suffering of those involved in various accidents. It gives counselling to the accidents victims and information as to where they can get assistance be it legal or humanitarian.
Health blogs
eXTReMe Tracker