Monday, February 23, 2009

AJALI YAUA SITA IRINGA

Mapema leo katika "Breaking News" nilitoa taarifa ya ajali ya basi la Hekima lililoua watu 6. Ifuatayo ni Taarifa kamili ya ajali hiyo kama ilivyoripotiwa na Francis Godwin katika gazeti la Tanzania Daima la leo.
Jinamizi la Ajali za barabarani, linaendelea kuliandama taifa, baada ya jana ajali nyingine iliyohusisha basi la abiria la Hekima, kugongana uso kwa uso na lori la mafuta na kusababisha vifo vya watu sita papo hapo na kuwajeruhi wengine 20.
Miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni pamoja na dereva wa basi hilo na utingo wa lori ambao hata hivyo majina yao hayakuweza kupatikana mara moja.
Mashuhuda wa ajali hiyo waliiambia Tanzania daima kuwa basi hilo lenye namba za usajili T 402 AM, mali ya Kampuni ya Hekima lilikuwa likitokea Tunduma, Mkoani Mbeya kwenda jijini Dar es salaam.
Baadhi ya abiria walionusurika katika ajali hiyo na ambao wamelazwa katika hospitali ya mkoa mjini hapa, walisema kwa nyakati tofauti kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori la mafuta kutaka kuyapita malori mengine mawili bila kujali basi hilo ambali lilikuwa likija mbele yake.
Majeruhi hao, Gibon Kajingili(25) na Raban Ngogo(23) wote wakazi wa mbeya, walisema dereva wa basi hilo alijitahidi kulikwepa lori hilo lakini ilishindikana na hivyo kugongana nalo uso kwa uso."Kama si uhodari wa dereva wa basi la Hekima kujitahidi kulikwepa lori hilo, huenda idadi ya vifo ingekuwa kubwa zaidi", alisema Ngogo.
Mkazi mmoja wa eneo wa eneo la ajali, Baton Ntuli, ambaye alifika na kumwokoa mmoja kati ya abiria aliyekuwemo katika basi hilo, Yules Nauli Sanga, alisema bada ya kufika eneo hilo wananchi walikuwa wakiendelea kuokoa majeruhi katika basi hilo na huenda kukawa na idadi kubwa ya watu waliopoteza masiha.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk. Oscar Gabone, alisema hadi majira ya saa 12 jana jioni, alikuwa amepokea majeruhi mmoja aliyefikishwa hospitalini hapo ambaye hata hivyo alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Alisema abiria watano ndio waliopoteza maisha katika ajali hiyo, akiwemo dereva wa basi na utingo wa lori ambao hata hivyo hakuweza kupata majina yao mara moja.
Kamanda Nyombi alisema katika ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 9.45 alasiri, abiria 15 ndio waliojeruhiwa na wako katika hali mbaya na wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Pia alisema majina ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo bado hayajatambuliwa na kuwa miili yote imehifadhiwa katika hospitali hiyo ya Mkoa na kazi ya utambuzi ilianza mara moja jana.
Hata hivyo alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori la mafuta ambaye alitaka kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele pasipokuzingatia sheria za usalama barabrani.
Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Dk. Athumani Mfutakamba, alisema kuwa jali hiyo ni mbaya kutokea katika wilaya hiyo ya Kilolo mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Saidi, alikuwa miongoni mwa viongozi wa serikali kusaidia kuwaokoa majeruhi hao.
HOJA: Jamani watanzania, hadi lini tutazidi kusikia habari za vifo kutokana na ajali zilizosababishwa na uzembe kama hii? wadau mjadala upo wazi.

No comments:

Post a Comment

This blog gives information about accidents-vehicles,motorcycles,bycycles etc,also highlights the suffering of those involved in various accidents. It gives counselling to the accidents victims and information as to where they can get assistance be it legal or humanitarian.
Health blogs
eXTReMe Tracker