Monday, February 16, 2009

TRAFIKI HAWAJAMUELEWA WAZIRI MKUU PINDA


Ifuatayo ni makala iliyoandikwa na Flora Wingia,mwandishi wa gazeti la Nipashe la Februari 15, 2009 katika safu ya maoni. kwa kuzingatia kwamba moja kwa moja inahausu suala kupunguza ajali nadhani ni ema tukaiweka hapa ili wadau wanaohusika na masuala ya ajali na jamii kwa ujumla wakapata ujumbe mzuri kutoka katika makala hii.

Flora ameanza kwa kuandika;

"Akiahirisha Mkutano wa 14 wa Bunge kule Dodoma wiki hii Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na mambo mengine amelishikilia bango suala la ajali za barabarani ambazo bado ni tishio kwa maisha ya watu na mali kupotea wkati zinaweza kuzuiwa kwa kiwango kikubwa.

hakuna mtu asiyetambua jinsi taarifa nyingi kuhusu ajali za barabarani zinavyoripotiwa karibu kila siku katika miji yetu mbalimbali. na katika ajali hizi, maisha ya watu wasiokuwa na hatia yamekuwa yakipotea huku wengine wakibakia na vilema ya kudumu, achilia mbali uharibifu wa vyombo vyenyewe vya usafiri.

miongoni mwa vyanzo vya ajali hizi ni pamoja na mwendo wa kasi, madereva wasio wazoefu katika uendeshaji wa magari, madereva walevi na pia vyombo vyenyewe kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kadhalika.

kwa upande mwingine, ajali hizo pengine kwa kiasi kikubwa zingeweza kuepukwa ikiwa polisi wa usalama barabarani wangetimiza wajibu wao ipasavyo.
baadhi ya madereva wamekuwa wakijiona kuwa hakuna anayweza kuwagusa na zaidi pale wanapotoa rushwa kwa baadhi ya polisi wetu wa usalama barabarani baada ya kuvunja sheria.
Wakati akifunga kikao cha Bunge wiki hii, Waziri Mkuu Pinda alivilaumu vyombo vya dola kwa kutosimamia sheria zilizopo zifanye kazi kikamilifu na hivyo kuwapa mwanya madereva kufanya vile watakavyo.
kwa mfano, alisema alikataza matumizi ya majani, mawe na magogo, kama alama ya kuonyesha kuharibika kwa gari, na badala yake vitumike viakisi mwanga(triangle reflectors)pembetatu.
pamoja na agizo hilo, lakini hadi leo hii, bado vitu hivyo vinaonekana barabarani pale gari linapoharibika. Matokeo yake, ajali nyingi zimeonekana kutokea katika eneo lenye alama hizo badala ya reflectors.
wanaopaswa kuhakikisha alama sahihi za barabarani zinakuwepo na zinazingatiwa ni trafiki wetu. Hawa wamepewa uwezo wa kuchukulia hatua za kisheria watakaobainika kuweka majani kama ishara ya tahadhari.
lakini swali ni je, kwanini hili hawalisimamii ipasavyo? Wamemuelewa Waziri wetu Mkuu? Kwa tafakari yangu nadhani bado hawajamuelewa. Kama wangemuelewa, uchafu huo unaowekwa barabarani ambao umechangia kutokea ajali nyingi na kwa muda mrefu sasa ungekuwa umeshaondolewa kitambo.
Wakati nalazimika kuungana na waziri mkuu kuwalaumu trafiki wetu kwa uzembe huo, lakini pia niiulize serikali yetu, kwamba je, polisi wa usalama barabarani wanazo nyenzo za kutosa kuwawezesha kusambaa sehemu mbalimbali katika umbali fulani wa barabara zetu ili kufuatilia nyendo za madereva wawapo safarini?
Hawa wanahitaji maari ya doria ili kuweza kuwanasa madereva wanaovunja sheria na kanuni za barabarani. pia wanapaswa kulipwa mishahara toshelezi kuwafanya waepuke vishawishi vya kudai chochote(rushwa) toka kwa madereva ili kuficha wavunjifuwa sheria na kanuni za usalama barabrani. Pengine haya yanaweza kusaidia kuwapa motisha mapolisi wetu watekeleze wajibu wao kwa ari na uadilifu. Vinginevyo, ajali zitaendelea kutikisa nchi huku nguvu kazi muhimu ikiendelea kutoweka.
katika angalizo, Waziri Mkuu ametoa takwimu kwamba mwaka jana kulikuwa na ajali za barabrani 20,148 ikiwa ni wastani wa ajali 55 kila siku au ajali 1,679 kwa mwezi na kusababisha jumla ya vifo vya watu 2,924 na kujeruhii wengine 17,825.
kwa Januari mwaka huu, akaongeza kuwa kulitokea ajali 252 ambazo zilisababisha vifo 185 na majeruhi 387. Takwimu hizi hakika zinaogofya na ni muhimu hatua madhubuti zichukuliwe ikiwa ni pamoja na adhabu kali dhidi ya wahusika ili iwe mfano kwa wengine.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amependekeza pamoja na matumizi yaa viakisi mwanga, pia madereva wanaobainika kusababisha ajali wafungiwe leseni kwa kipindi kirefu na kama ni mara nyingi, basi wanyang'anywe kabisa leseni. hili hata mimi naliafiki ".
Hoja yangu:Makala hii ni muhimu na inabeba yale yote ambayo Waziri Mkuu alipendekeza ili kuhakikisha kwamba maisha na mali haviteketei kwa sababu ya uzembe wa madereva ambao hawathamini maisha ya binadamu wenzao. nathubutu kusema kwamba wanapoona binadamu mwingine amekufa haimshtui na labda anajisikia furaha. Kwanini? kwa sababu wengekuwa hawapo hivyo basi wangezingatia sheria na maadili ya kazi yao na kuokoa maisha na mali za watu. Kwa matrafiki hatuna jipya la uongeza, karibu yote yameshaongelewa, tusubiri kuona utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment

blogarama - the blog directory
Directory of News Blogs
This blog gives information about accidents-vehicles,motorcycles,bycycles etc,also highlights the suffering of those involved in various accidents. It gives counselling to the accidents victims and information as to where they can get assistance be it legal or humanitarian.
Health blogs
eXTReMe Tracker