Tuesday, April 7, 2009

AJALI ZA BARABARANI! A Poem.

Nipokee mhariri, japo niwe upenuni,
Niipange mistari, isomeke gazetini,
Lengo sineni stori, mtima una huzuni,
Ajali barabarani, nani apewe lawama.

Uianzapo safari, ya gari barabarani,
Hata waendao feri, roho zao mashakani,
Mwendo wao ufahari, waongozapo sukani,
Ajali barabarani, nani apewe lawama.

Tuwaite majangili,wa roho zetu jamani,
Madereva wa magari, wale wasio makini,
Wawabeza askari, wawapo barabarani,
Ajali barabarani, nani apewe lawama.

Nakaa na kufikiri,watenda kwa umakini,
Nionapo askari, redio zi mikononi,
Wazibaini ajali, hata zile pembezoni,
Ajali barabarani nani apewe lawama.

Leseni zenye mihuri, zimejaa mifukoni,
Vyuo vingi kushamiri,sawa nyanya sokoni,
Ujuvi kwao sifuri,waingiapo njiani,
Ajali barabarani, nani apewe lawama.

Naangaza na bahari, wapo watu safarini,
Manahodha ni mahiri, waongoza umakini,
Ajali hazishamiri, watu vyema gatini,
Ajali barabarani, nani apewe lawama.

Naufunga ushairi, japo ninazo huzuni,
Vipato kwa matajiri, sisi kwetu huzuni,
Twayapanga makaburi, ndugu jamaa jirani,
Ajali barabarani, nani apewe lawama.
(Elias S. Kitu,'Mwananchi')

No comments:

Post a Comment

This blog gives information about accidents-vehicles,motorcycles,bycycles etc,also highlights the suffering of those involved in various accidents. It gives counselling to the accidents victims and information as to where they can get assistance be it legal or humanitarian.
Health blogs
eXTReMe Tracker