Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Tanga imeanza kusikiliza kesi inayomkabili mmiliki pamoja na nahodha wa jahazi la Amana Pemba ambalo liliungua na baadaye kuzama baharini Aprili 14 mwaka huu.
Watuhumiwa hao,Ngwalu Haji Ali,43, na Sabiha Saleh Suleman 43,wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kushindwa kufuata kanuni na sheria za uendeshaji vyombo vya usafiri baharini, wakituhumiwa kukiuka kifungu cha 3 cha sheria ya mwaka 2003 kwa kuliruhusu jahazi hilo kuondoka bila kibali cha Mamlaka ya Bandari Tanga.
Washtakiwa hao pia wanadaiwa kusababisha ajali ya kujeruhi watu huku baadhi wakihofiwa kufa.
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Magdalena Nason, mwendesha mashtaka wa serikali, Inspekta Genes Tesha alidai kuwa mnamo April 14 mwaka huu, majira ya saa 4 usiku mshtakiwa wa kwanza, amaye ni nahodha wa jahazi lenye namba za usajili Z733 aliondoka bila kufanyiwa ukaguzi na vyombo vya usalama majini.
Ilidaiwa kuwa siku ya tukio mtuhumiwa huyo, Ngwalu Haji Ali alishindwa kufuata kanuni na maelekezo ya kibali cha umiliki wa jahazi hilo uliomtaka kubeba abiria 10 lakini badala yake alipakia abiria zaidi ya 60.
Washtakiwa hao wote wawili wamekana mashtaka hayo na wako nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana iliyotaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini au kwenye taasisi zinazofahamika na kusaini dhamana ya sh. 1 milioni.
Mwendesha mashtaka huyo wa polisi alidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba kesi hiyo itatajwa tena Mei 4 mwaka huu (Source:Mwananchi).
No comments:
Post a Comment