Ni juzi tu kijana Lazaro(23) dereva wa taksi maeneo ya Suka Kimara, alipigwa risasi kwa kushukiwa kwamba ni jambazi jambo ambalo wakazi wa eneo hilo wamelipinga na kuwa na hisia tofauti.
Kama wanavyodai polisi kwamba siku hiyo eneo hilo kulikuwa na tukio la ujambazi na hivyo walishuku kwamba alihusika katika tukio hilo.
Katika hali ya kawaida, inatokea ghafla unaona watu wenye silaha wanakusimamisha wakitokea vichakani, je utasimama?maana hawana sare za polisi , wamevaa kiraia na wanaelekeza mtutu wa bunduki kwako. Nadhani kwamba aidha utakimbiza gari au utasimama kwa hofu kubwa ukijua kwamba sasa mambo yameishaharibika kutokana na hofu kwamba majambazi yameishakuteka!
Jeshi la Polisi linatumia nguvu na muda mwingi kuwaelimisha wananchi juu ya "Polisi-Jamii" lakini inaonekana wanasahau wajibu wa kutengeneza "Client Service charter" yaani mkataba kati ya 'mpokea' na 'mtoa' huduma. Polisi wanatakiwa kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kufanya kabla ya kutegemea wananchi watekeleze wajibu wao.
Kwa mfano, askari anapomkamata raia au tuchukulie mfano askari aliyemmiminia risasi kijana Lazaro, wakati anamsimamisha alikuwa ametimiza wajibu wake? Je, alikuwa ana kitambulisho chochote cha kumfanya Lazaro asiwe na hofu kwamba anasimamishwa na majambazi?
Tunaona nchi za wenzetu hata katika senema, kitu cha kwanza askari anachofanya ni kutoa kitambulisho chake na hata kujitambulisha kwa mayowe "Police! police!" Wengine huvaa vitambulisho vyao kama mkufu unaning'inia shingoni-hii yote ni kumtoa hofu anayesimamishwa ajue anasimamishwa na watu wema, walinzi wa usalama. Hapo askari anakuwa amekamilisha majukumu yake katika "Client Service Charter".
Mashuhuda wanasema kijana Lazaro alihofu kufungua dirisha lote na akashusha dirisha kidogo, lakini askari wakafanya waliyofanya.
Ni lazima kufahamu kwamba kijana Lazaro alikuwa anaendesha gari jipya na historia inaonyesha kwamba katika maeneo hayo ya Suka na Temboni kuna madereva ambao waliishatekwa na kunyang'anywa magari.
Najiuliza, je kulikuwa na uwezekano wa askari hao kutoboa magurudumu ya gari ili asiweze kukimbia kuliko kumpiga risasi?
Nakumbuka tukio lililompata kaka yangu yapata miaka 6 au 7 hivi iliyopita. Alikodi teksi eneo la njia panda ya whitesands kwa nia ya kupelekwa nyumbani kwake Salasala. Mara wakaona gari ya polisi maarufu "ki-gofu" ikiwafuata kwa kasi, askari 'wakikoki' bunduki zao(SMGs) tayari kushambulia. Kisa? walidai ati walikuwa wanaenda kufanya ujambazi.Mungu saidia, dereva hakushtuka akasimamisha gari. Na kwakuwa walikuwa na sare za polisi kidogo ilileta imani kwamba ni walinda usalama japo majambazi mengine huvaa sare za polisi. Baada ya hapo walipelekwa Oysterbay Police na kugundulika kwamba gari waliyokuwa wanaifuatilia siyo yenyewe. Lakini kumtoa hapo kituoni nadhani wadau mnajua kasheshe yake.
Ni kwa mifano kama hii,ndiyo maana nasema "kwa mtindo huu wengi tutauawa". Askari wawe na vitambulisho popote pale, maana wakivaa kiraia kama raia mwingine yoyote na silaha mkononi nani atajua wao ni watu wema hasa ikiwa katika mazingira tatanishi?
Nafikiri dhana ya "Polisi Jamii" ni nzuri lakini mapungufu kama haya yatupiwe macho.
NAWASILISHA!
No comments:
Post a Comment