Technograph haiwezi kunusuru maisha ya watu.
Hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ikishirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi Cha Usalama Barabarani wametangaza amri kuwa wamiliki wa mabasi ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo magari yao yawe yameweka mikanada kwenye kila kiti na chombo kinachoratibu mwendokasi wa gari (Technograph).
Amri hii imeshangaza wengi na darubini kuanza kumulika na kujiuliza kama wenye dhamana ya kuamua mambo kama haya wana dhamira ya dhati ya kuingiza teknolojia mpya ili iweze kumsaidia na kulinda maisha ya watanzania au nao ni mateka wa wale wanaotaka kuigeuza nchi yetu kuwa jalala la kutupia vitu vilivyopitwa na wakati.
kama si mateka wa hilo, basi kuna wajanja wamebuni mradi wa kujipatia fedha wa kuuza vifaa hivyo kwa visingizio vya kuingiza teknolojia mpya kudhibiti ajali kwa kisingizio cha kunusuru maisha ya wananchi na maliz zao. Na mara nyingi zoezi kama hili hufanyika kama si mwanzo wa muhula wa utawala basi huwa mwishoni mwa muhula.
Amri hii ni ushahidi mwingine unaoonyesha kuwa licha ya nchi yetu kuwa na wasomi katika kila sekta lakini wasomi hao ama wamestaafu kufikiria au hawasomi na kufuatilia mambo mapya yanayoweza kuisaidia kuleta ufanisi. Matokeo yake wanadhani kutoa amri zilizopitwa na wakati zitawafanya waonekane ni wachapa kazi na wana uchungu na nchi.
Mwaka 1996 kulipozuka mvutano kati ya serikali na wamiliki wa mabasi juu ya kufunga vidhibiti mwendo, wamiliki wa mabasi walipendekeza badala ya kufunga vidhibiti mwendo, kifungwe chombo kinachoonesha mwendokasi wa safari nzima ya basi hizo(technograph) lakini serikali kwa ubabe ilikataa ushauri huo na kulazimisha ule wake.
Leo miaka 13 imepita tangu serikali ikatae pendekezo la kufunga chombo cha technograph kwa madai kuwa vidhibiti mwendo vimeshindwa kuzuia ajali. Serikali hiyo hiyo sasa inaamrisha kufungwa kwa technograph teknolojia ambayo sasa imeshapitwa na wakati na haiwezi tena kudhibiti ajali wala kukisaidia chombo chochote cha dola zaidi ya mmiliki.
Kwa faida ya wasomaji technograph ni chombo kinachofungwa kwenye gari na funguo hubaki kwa mwenye basi. Gari linapokwenda safari na kurudi mmiliki hufungua chombo hicho na kutoa kadi inayoonyesha mwendokasi wa gari kwa safari yote. Polisi wa Usalama barabarani hawezi kufungua chombo hicho njiani kwa vile funguo zipo kwa tajiri.
Chombo hicho ni kama kile cha kwenye ndege kiitwacho 'kisanduku cheusi' ambapo hadi ajali itokee ndipo hutafutwa ili kujua kipi kilichosababisha ajali, ni mwendokasi au vipi? Sasa chombo hicho imeamriwa kifungwe ndani ya miezi 6 tu muda huo ni mfupi hata kwa wasimamizi wa sheria barabarani kujiandaa kujua namna ya kusoma chombo hicho.
Kinachoshangaza, vyombo vinavyosimamia sheria na taratibu za usafiri wa nchi kavu na majini, wanapaswa kwanza kufanya utafiti wa kina kabla ya kuja na amri mpya ambazo haisaidii kutatua matatizo ya usafirishaji zaidi ya kuongeza gharama za uendeshaji na hivyo serikali kushindwa kuwalinda wawekezaji wa sekta hii ambao wengi ni wazalendo.
Wakati SUMATRA na polisi wanafikiria kufungwa kwa chombo kilichopitwa na wakati cha technograph, baadhi ya kampuni hapa nchini sasa zinatumia mfumo mpya kabisa wa kudhibiti mwenendo wa mabasi ujulikanao kama fleet management system au tracking system unaounganishwa kwenye mtandao hutoa ripoti hapo hapo.
Basi hufungwa chombo kinachofanana na flashi ya kompyuta. Kila dereva ana namba yake ya siri. Endapo kutakuwa na dereva hana namba ya siri lakini akataka kuliendesha basi hilo halitawaka abadani. Chombo hicho kina uwezo wa kuonesha basi hilo lipo wapi, linakwenda mwendokasi upi na hali ya hewa ikoje hapo lilipo kila baada ya dakika mbili.
Chombo hicho huonyesha hata makosa ya kiutaalamu yaliyofanywa na dereva na muda aliofanya kosa hilo endapo mtandao wa GSM ukienea nchi nzima. Mtandao huu unaweza kulionesha basi hilo muda sawia na hapo lilipo kwenye runinga ya kompyuta. Teknolojia hii ingekuwa sahihi kutumika na polisi na SUMATRA kwa sasa.
Kumekuwapo na vikao vya mara kwa mara na wadau kuhusu uboreshaji wa sekta ya usafiri lakini vikao hivi vinaonesha ni kiini macho cha waliokabidhiwa dhamana ya usimamizi na uboreshaji wa sekta hii ili kuhalalisha mambo wanayodhani yana maslahi kwao zaidi kuliko pande zote zinazohusika yaani Mwnachi, serikali na mwekezaji.
Amri kalikali zinapotolewa na zisipofanya kazi ndipo wahusika huanza kufikiria kuwatafuta wadau na kuketi nao kujadili tatizo, ni vizuri wadau wakahusishwa kabla ya uamuzi kufanywa na pia wadau hao wakashirikishwa pia katika maandalizi kabla amri hiyo kuanza kutekelezwa ni dhahiri technograph haitasaidia kudhibiti ajali.
Mamlaka za usafiri nchini Kenya ziliamua tangu mwaka 2003 kila basi linalobeba abiria hadi matatu (hapa kwetu daladala) kila kiti kiwe na Mkanda wa usalama wa abiria.
Wametekeleza kwa nguvu zao zote hadi mabasi ya watanzania yafanyayo safari zake huko yametekeleza amri hiyo na kila abiria abiria anatekeleza amri hiyo kwa umakini.
Hapa nchini yapo mabasi yenye mikanda lakini abiria kila wanapoambiwa kufunga mikanda hiyo hudharau.
Hakuna sheria inayowabana abiria, endapo kungekuwepo na sheria inayowabana abiria kama ilivyo huko Kenya abiria akikutwa hakufunga mkanda hutozwa faini ya shilingi 500 za nchi hiyo la sivyo mikanda hiyo itakuwa mapambo (Habib Miradji, Mwananchi Machi 8).
HOJA: Nimekutana na hii makala ambayo nilionelea ni vema wasomaji wangu wakapata ladha kama niliyoapata mimi na kuweka mjadala wazi ili tuchangie na kuona ni jinsi gani labda mamlaka husika zitazinduka na kujua kwamba Tanzania ya sasa sio ya mwaka 47. Watanzania wapo macho!!!
No comments:
Post a Comment